Thursday, June 28, 2012

Vazi Lililotobokatoboka

by Tyson jacob

Katika Biblia, kuna watu ambao walifundishwa habari za Injili ya Yesu Kristo, wakazingatia mafundisho yale. Baada ya kuyazingatia, wakaanza kuyaishi hivyo wakafanyika WANAFUNZI wa Yesu, kweli kweli. Watu ambao hawakuwa wamejifunza habari za Injili, walipoona jinsi wanavyoishi wale Wanafunzi wa Yesu, walishangaa sana kwa kuwa walikuwa wanaishi sawa sawa na walivyofundishwa, na maisha yao yalibadilika yakafanana na Kristo. Jambo hili liliwafanya, wale wanafunzi, waitwe WAKRISTO. Walikuwa wamelivaa Vazi la Ukristo. Ukristo ikawa ni Matokeo ya Vile mtu alivyo.

Miaka iliendelea, Watu wakiwa wanaitwa Wakristo, kutokana na vile walivyokuwa wanaishi. Mwenendo wa maisha yao uliwatetea na kuwatambulisha kwa jamii inayowazunguka kuwa wao ni Wakristo. Lakini kadri miaka ilivyozidi kusonga ile hali ya mtu Kuitwa Mkristo kutokana na alivyoishi nayo iliendelea kubadilika. Kukatokea watu ambao pamoja na Kuitwa waKristo, lakini walianza kutenda mambo ambayo yanatofautiana na mafundisho ya Kristo. Hali hii ilisababisha baadhi ya watu kutumia “Ukristo” kama njia moja wapo ya kujitetea kuwa Yeye ni “Mtu mwema”.

Katika siku zetu, hata sasa unaposoma maneno haya, kuna mahali kuna mtu ambaye anajiita Mkristo lakini anatenda tofauti na Mafudisho ya Kristo. Miaka kadhaa iliyopita, wakati badiliko hili la Ukristo kutoka katika kuwa Matokeo ya mtu anavyoishi na kuwa ni Mtu anayetazamiwa kuwa hivyo, Wachungaji wengi waliibiwa na kupoteza malizao nyingi kwa kuwa watu walikuwa wanajitambulisha kuwa yeye ni Mkristo, kwa hiyo anahitaji msaada wa kulala japo kwa usiku huo tu ili kesho aendelee na safari yake. Na mtu akipewa hifadhi alikuwa anatumia mwanya huo kuiba na kutokomea kabla jua halijachomoza. Vazi la Ukristo likawa limetobolewa tobolewa. Ikawa ni lazima mtu avae vazi jingine ndani ya vazi hilo ili kukinga yale matundu ya vazi la Ukristo.

Baada ya kuona hivyo, wale walioendelea kuishi kwa kadri ya Mafundisho ya Yesu, ilibidi waweke vazi jingine ndani ya Vazi la Ukristo. Wakawa wanaitwa kuwa Mtu aliyeokoka. Kwamba kule kusema tu ni Mkristo ikawa haitoshi tena, ni lazima kuwe na kingine zaidi ya hapo. Wakawepo Wakristo Waliookoka. Ndani ya Wakristo wakawepo Wakristo wanaoishi kidunia kabisa na Wale wanaoishi Kikristo. Hivyo kukaja na Vazi jipya la “Kuokoka”.

Miaka imekwenda, huku vazi la Kuokoka likiwa linatumika kuziba yale matundu ya Ukristo, lakini inaonekana kuwa Vazi la “Kuokoka” nalo linaonekana Kuchakaa,na pengine tayari limeshaanza kutoboka. Kule kusema mtu “ameokoka” nayo inakuwa tu ni mtu anayetazamiwa kuwa hiyvo! Wengi wametapeliwa kwa jina la “kuokoka”. Wasichana na wavulana wengi wamejikuta katika misiba ya ndoa kwa kuwa wakati wa uchumba, mmoja wapo alivaa vazi la Ukristo lililotoboka, kisha akavaa na vazi la ‘Kuokoka” ambalo nalo kumbe limetoboka pia….! Na mifano mingine mingi ya yakuonyesha jinsi hali hii ilivyo.

Nimetafakari, nimewaza sana kuwa baada ya hivi vitambulisho viwili, au mavazi mawili kutobokatoboka, yaani Ukristo na Kuokoka kutokutosheleza kuwa ni Jina la Mfuasi wa Kristo, ni jina gani jipya litafuatia baada ya haya mawili? Ikiwa wakristo wa kwanza, waliookoka katika mapambazuko ya Injili, walistahili Kuitwa Wakristo kwa kuwa waliishi kama Kristo alivyofundisha, nadhani bado kuna uzuri kwa Wafuasi wa Kristo kutambulika katika jamii inayowazunguka kwa kuwa Ni Mabalozi wa Kristo. Je, hao wanatambulika au watatambulika kwa jina gani jingine?

Naendelea kuwaza.....

Maandiko ya rejea: Mdo 11:26; Lk 11:39; Math 23:25-28


No comments:

Post a Comment